Katika tukio lisilo la kawaida, wananchi waliokuwa katika mnada wa Dosidosi wilayani Kiteto Mkoani Manyara walimshambulia kwa silaha za jadi askari polisi aliyetajwa kwa jina la PC Ginue wa kituo cha Polisi Kibaya, kisha kumpora bunduki aina ya SMG na kutokomea nayo.

Tukio hilo lilitokea JAN baada ya polisi huyo aliyekuwa na silaha kumuokoa mtu mmoja aliyekuwa akishambuliwa na wananchi hao kwa tuhuma za kupora shilingi 800,000 kutoka kwa mmoja wa wafanyabiashara waliokuwa mnadani hapo.

Shuhuda wa tukio hilo alieleza kuwa askari huyo aliyekuwa katika mnada huo kwa lengo la kuimarisha usalama alilazimika kupiga risasi hewani wakati wananchi hao wakimshambulia mtuhumiwa na kufanikiwa kumuokoa kabla askari wenzake kufika na gari na kumchukua mtuhumiwa huyo.

Hata hivyo wakati wanaondoka na gari, askari huyo alichelewa kupanda katika gari na kuishia mikononi mwa wananchi hao waliokuwa na hasira kali.

“Wakati askari hao wanaondoka na gari hilo wakiwa na mtuhumiwa, PC Ginue alichelewa kupanda gari hilo, kwa hiyo wananchi walimvamia na kuanza kumshambulia kwa fimbo na silaha za jadi. Walipofanikiwa kumzidi nguvu, walimpora bunduki na kutokomea nayo kusikojulikana,” shuhuda huyo alimwambia mwandishi wa gazeti la Mtanzania.

Mkuu wa wilaya ya Kiteto, Samuel Nzoka alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kulilaani akiwataka wananchi waliopora silaha hiyo kuirejesha. Pia, aliwataka wananchi wema kushirikiana na Jeshi la Polisi ili bunduki iliyoporwa ipatikane.

“Hili halikubaliki hata kidogo, yaani raia anamnyang’anya askari silaha laki kama SMG! Hivi aliyeichukua anaipeleka wapi, wairudishe haraka kwa sababu lazima watapatikana tu,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Gazeti la Mawio Lapigwa 'Kifungo cha Kudumu'
Baba amng'ata mwana kama Paka akimfunza asiwe 'Shoga'