Afarah Suleiman, Babati – Manyara.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja amewataka Wananchi wa Mkoa huo na watanzania kwa ujumla, kujenga tabia ya kupanda mlima Hanang unaopatikana katika Wilaya hiyo.
DC Mayanja ameyasema hayo wakati aliposhiriki zoezi la kupanda mlima huo, lililoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS, la Hifadhi Mazingira Mlima Hanang, na kuongeza kuwa litasaidia Vijana kujifunza, kutunza na kulinda mazingira.
Aidha Mayanja pia ametoa vyeti kwa Vijana zaidi ya 550 kutoka katika maeneo mbalimbali ya Mkoa Manyara, ambao wamepanda na kufika kileleni katika mlima huo wa nne kwa urefu Tanzania, huku akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa kutunza na kulinda mazingira katika hifadhi hiyo.
Kwa upande wake Afisa Utalii katika Hifadhi hiyo, Elizabeth Mbunda, amesema kutokana na juhudi mbalimbli za Serikali kwa Kushirikiana na Watumishi wa TFS kuwahimiza na kuona umuhimu wa kutembelea Hifadhi, kwasasa muitikio wa Wananchi umekuwa mkubwa ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.
Amesema, wenyeji wa Wilaya hiyo hasa wanaouzunguka mlima huo walikuwa wakiuona mlima huo kama pori la kawaida lakini baada ya Serikali kuboresha Miundombinu na TFS kutoa Elimu na hamasa sasa wamekuwa mabalozi wakubwa .
Mbunda ameongeza kuwa, hifadhi ya mlima Hanang ni zaidi ya Utalii wa Ikolijia wa Mazingira, kwani kuna mimea inayopatikana humo pamoja na Kinyonga ambaye anapatikana kwa upekee ndani ya Mlima Hanang .
Amesema, zoezi hilo la kupanda mlima hufanyika Oktoba 14 kila mwaka, katika siku ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, lakini mwaka huu hawakuweza kufanya hivyo kutoka na tukio kubwa la kuzima mwenge wa Uhuru Kitaifa kufanya mkoani humo na kwamba gharama ni nafuu inayozingatia hali ya Mtanzania.