Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amepongeza wadau kwa juhudi za kuhifadhi mazingira na kuonesha nia ya kufanya Biashara ya Kaboni nchini.
Jafo ayamesema hayo alipokutana na Meneja wa Shirika linalohudumia wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) la Denmark Bi. Jo Povey katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma leo Juni 14, 2023.
Amesema, Serikali inatambua juhudi za wadau hao ambao wanafanya shughuli za kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti katika kambi za wakimbizi zilizopo mkoani Kigoma na wananchi wanaozunguka kambi hizo na kwamba Serikali inaendelea kuzifanyia kazi Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni ili wananchi wanufaike na biashara hiyo.
Waziri Jafo amesema changamoto ya ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa ni ni kubwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini hali inayochangia uharibifu wa mazingira na ukame na kusababisha upungufu wa maji na chakula na kuwashukuru wadau hao kwa kuonesha nia ya kuwekeza katika nishati mbadala ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
“Tunafurahi tunapoona wadau kama ninyi mnashiriki kikamilifu katika kulinda mazingira na tunaona juhudi zenu zE kupanda miti, kutuletea nishati mbadala na kuona namna ya kusaidia katika uwekezaji wa hewa ya ukaa na kwa upande wetu kama Serikali tunaendelea kuhamisha wananchi wahifadhi
mazingira,“ amesema.
Kwa upande wake Meneja wa shirika hilo Bi. Jo amesema kipaumbele chao tangu mwaka 2021 ni kushirikiana na Serikali katika suala la upandaji wa miti ili kuhifadhi mazingira na kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) pamoja na Halmashauri ya Kibondo mkoani Kigoma wanapanda miti katika kambi za wakimbizi na maeneo ya jirani ili kurudisha hali ya mazingira iliyokuwepo awali.