Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtaka Naibu wake William Ruto, kuacha kueneza uongo kwa Wakenya kwamba alimtendea mabaya wakati wa uongozi wake.
Rais Kenyatta, ameyasema hayo wakati akiindua miradi ya miundomsingi katika Kaunti ya Mombasa Agosti 4, 2022, na kusema Kenya haina haja na kiongozi anayewahada.
Kauli ya Kenyatta, inakuja kufuatia madai ya Ruto kwamba Serikali ya Jubilee, ilifeli katika muhula wake wa pili, kwa kushindwa kukamilisha miradi ya maendeleo, kufuatia kumalizika kwa tofauti kati ya Rais huyo na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.
“Raila ndiye anayefaa kuwa mrithi wangu, na ninamshauri Ruto kusubiri fursa nyingine ya kuwania urais lakini si sasa maana Wakenya wanahitaji kutafutiwa suluhu ya matatizo na sio maneno,” amesisitiza Rais Kenyatta.
Amesema, “Ninasikia wakisema kwamba miradi ya serikali ilikamilika mwaka wa 2018 wakati wa handshake na kakangu Raila wacha niwaulize, huu mradi tunaouzindua leo, tulizindua 2020, sasa ilikuwa ni baada au kabla ya handshake?.”
Aidha ameongeza kuwa, “Kwani hii sio kazi tumefanya? Tunahitaji Serikali itakayowaunganisha Wakenya wote, kwa hiyo tumruhusu Raila aingie ili aweze kufanya kazi, wengine wasubiri fursa nyingine wakati mwingine.”
Katika hatua nyingine, Naibu Rais wa Kenya, William Ruto amemtaka Mkuu wake Rais, Uhuru Kenyatta kuhakikisha kuwa taifa liko salama wakati huu wa uchaguzi mkuu, kwa kutuliza wanaopanga kuzua chuki za kisiasa.
Ruto amesema, baadhi ya maafisa wa Serikali wanafanya siasa zisizofaa kwa kumnadi mgombea wa Azimio Raila Odinga, huku akisema Serikali ikubali kuwa Raila hawezi kushinda uchaguzi wa urais na kwamba Wakenya wataamua nani anafaa kuliongoza Taifa hilo.
“Ile wasiwasi tunaona Azimio haitawasaidia na kile tunamuomba Rais, kwa heshima, ni asiruhusu nchi kupatwa na chuki za kisiasa hata kama project yake imeanguka. Hakuna haja ya kuanza kueneza chuki,” amesema Ruto.
Kenya, inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu Agosti 9, 2022, ili kumpata mrithi wa Rais wa sasa Uhuru Kenyatta, ambaye ameliongoza Taifa hilo kwa mihula miwili.