Serikali nchini, imeendelea kuimarisha sekta za maliasili na utalii, kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali ili kukuza utalii, kuitangaza nchi yetu na vivutio vyake kitaifa na kimataifa pamoja na kuimarisha mchango wa sekta hizo kwenye pato la Taifa.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na kuongeza kuwa katika mwaka 2022/2023, programu mbalimbali zimeendelea kutekelezwa ikiwemo ya Tanzania – The Royal Tour na utangazaji wa vivutio vya utalii, kupitia matukio mbalimbali na vyombo vya habari ikiwemo Tanzania Safari Channel.

Amesema, “kutokana na jitihada hizo, idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka watalii 922,692 katika mwaka 2021 hadi kufikia watalii takriban milioni 1.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 57.7. Vilevile, idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 199.5.

Aidha, Waziri Mkuu pia amesema Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuwa bora duniani ambapo kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2022 imepata tuzo ya dhahabu ya utoaji wa huduma bora huku akisema kwa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ina changamoto ya ongezeko la watu, mifugo, makazi holela na shughuli za kibinadamu hivyo kukosekana kwa uwiano baina ya uhifadhi, ukuzaji wa utalii na maendeleo ya jamii.

Mwakinyo apata sapoti, Milioni 35
Hizi hapa ndoto za Frank Lampard