Uingereza, imeanza ukurasa mpya wa kujitegemea kutoka umoja wa Ulaya, baada ya usiku wa kuamkia Januari Mosi kukamilisha rasmi safari ya kujitoa kwenye umoja huo.

Uingereza, iliacha kufuata sheria za umoja wa Ulaya kuanzia saa sita usiku kuamkia Ijumaa, ambapo sasa itakuwa na sheria zake za kusafiri, biashara, uhamiaji na usalama.

Waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, amesema “uhuru uko mikononi mwao” na kuwa na uwezo wa “kufanya vitu tofauti na kwa namna bora”, akisema mchakato wa muda mrefu wa kujitoa umekamilika.

Licha ya hatua hii, wanasiasa na watu waliopinga nchi hiyo kujitoa umoja wa Ulaya, wanasema hali itakuwa mbaya zaidi.

Waziri wa kwanza wa Uscotishi, Nicola Sturgeon, ambaye mara zote amekuwa akitaka nchi yake kubaki kwenye umoja wa Ulaya, amesema kupitia ukurasa wake wa kijamii wa twitter “Scotland itarejea karibuni kwenye umoja wa Ulaya, kuweni na imani”.

Mawaziri wa Uingereza, wameonya kuhusu uwezekano wa kushuhudiwa sintofahamu katika baadhi ya mambo, wakati huu taifa hilo likitekeleza sheria zake tofauti na zile za umoja wa Ulaya.

Rais Mwinyi abadilisha uteuzi alioufanya
Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar ala kiapo