Mahakama ya Uingereza imekataa ombi la Marekani la kumuhamisha mwanzilishi wa mtandao wa WikiLeaks Julian Assange, hadi nchini Marekani anapokabiliwa na mashtaka ya ujasusi.
Mahakama imesema kuwa hatua ya kumuhamisha Assange, ni ukandamizaji kutokana na afya yake ya kiakili na kuongeza kuwa Assange huenda akajiua iwapo atahamishwa hadi Marekani.
Hata hivyo, serikali ya Marekani imesema itakata rufaa juu ya uamuzi huo.
Waendesha mashtaka wa Marekani wanamshtumu Assange kwa makosa 17 ya ujasusi na matumizi mabaya ya Kompyuta kwa kuchapisha mtandaoni nyaraka za siri juu ya oparesheni za jeshi la Marekani nchini Iraq na Afghanistan muongo uliopita.
Iwapo atapatikana na hatia, Assange huenda akapewa kifungo cha miaka 175 jela.