Mradi wa Ujenzi wa Kingo za Bahari unaoendelea katika fukwe ya Ocean road katika Bahari ya Hindi Jijini Dar es salaam kwa ajili ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi unaendelea kwa kasi nzuri.
Hayo yamesemwa na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu.
Amesema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa vyoo na mabenchi ya kupumzikia, pia utakuwa na jumla ya urefu wa mita 860 kuanzia Hospitali ya Agha-Khani kupitia viwanja vya Ikulu.
“Ukiangalia kwenye fukwe zetu hazina vyoo, hivyo kuwafanya watu wanaokuja kupumzika kukosa sehemu za kwenda kujihifadhi, jambo ambalo sio zuri, ukizingatia Jiji letu linapokea wageni kutoka sehemu mbalimbali, ndio maana tumeamua kuleta mradi huu ili kuondoa aibu hii,”amesema Mwita.
Aidha, ameongeza kuwa maeneo ya kupumzikia katika Jiji la Dar es Salaam sio rafiki kutokana na ukosefu wa miundombinu hivyo kukamilika kwa mradi huo kutaondoa baadhi ya changamoto zilizopo kwenye maeneo ya hayo.
Hata hivyo, Katika hatua nyingine, Mwita amewasihi vijana waendelee kujitokeza kuchukua mikopo yenye masharti nafuu ambayo itawasaidia kujiendeleza kiuchumi.