Na Allawi Kaboyo- Bukoba.

Mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA Kagera unaotekelezwa na serikali ya China umeshindwa kukamilika kwa wakati uliopangwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ya Maji.

Taarifa iliyotolewa na msimamizi wa ujenzi na mwakilishi wa serikali ya Tanzania Mhandisi Frank Thomas, mbele ya Naibu Katibu mkuu wizara ya Maji imeeleza kuwa mradi huo ulitakiwa kukamilika mwaka huu lakini kutokana na changamoto za Corona pamoja na kutokuwepo kwa huduma ya Maji, umezorota.

Frank ameeleza kuwa wanalazimika kusomba maji wanayoyatumia katika ujenzi kwa magari kutoka kwenye mito midogo wakati uhitaji kwa siku ni Lita Elfu 50 hali ambayo inawapelekea kutumia gharama kubwa ya kusomba Maji na wakati mwingine kusababisha kazi kusimama.

Akijibu hoja hizo Naibu katibu mkuu wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba, ambaye amefanya ziara katika mradi huo, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuongeza kuwa Wizara inalitambua hilo na ndio maana amefika ili kuona namna ya kulimaliza tatizo hilo.

Kemikimba ameelekeza watendaji wa Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA), kuanza utekelezaji wa mradi huo wa Maji mapema mwezi Novemba na kuhakikisha ifikapo mwezi machi mwakani Maji yawe yamefika Chuoni hapo na kuanza kutumika.

Kemikimba ameendelea na ziara yake mkoani Kagera kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali ya Maji katika halmashauri za Manispaa ya Bukoba, Halmashauri ya wilaya Bukoba na Halmashauri ya wilaya Muleba.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Oktoba 13, 2020
Ujenzi treni ya umeme wapamba moto