Ujerumani imeongeza muda wa hatua kali za kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona hadi tarehe 31 Januari 2021.
Aidha Uamuzi huo umefikiwa baada ya kufanyika mkutano kati ya Kansela Angela Merkel na viongozi wa majimbo ya shirikisho.
Akitangaza hatua hizo Kansela Merkel amesema vikwazo vikali zaidi vitawekwa kuzuia mikusanyiko ya watu ili kudhibiti ongezeko la maambukizi.
Masharti yatakayotekelezwa nchini kote Ujerumani ni pamoja na kuendelea kuzifunga shule, biashara na huduma zote zisizo za lazima hadi mwishoni mwa mwezi Januari.
Masharti hayo ambayo yaliwekwa katikati mwa mwezi uliopita wa Desemba yalitarajiwa kumalizika tarehe 10 Januari.
Kansela Merkel amesema aina mpya ya virusi vilivyotoka nchini Uingereza, na msimu wa baridi vinaleta changamoto inayohitaji hatua kali za kukabiliana navyo.