Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo kwa nyakati tofauti wametuma ujumbe kuhusu uamuzi wa Rais John Magufuli kumsamehe Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye.

Jana, Nape alifika Ikulu jijini Dar es Salaam, akazungumza na Rais Magufuli na kueleza yaliyokuwa yanamsibu na mwisho akaondoka akiwa na furaha ya kusamehewa.

Makonda ametumia mtandao wa Instagram kueleza jinsi alivyofurahishwa na tukio hilo lililokuwa gumzo.

“Hakika Mungu ni mwema, moyo wa Baba ni kutulea watoto nami nimefurahi sana sana kumuona kaka yangu Nape akiwa na Baba. Sisi ni wa nyumba moja na siku zote tu wamoja,” aliandika Makonda akiambatisha video ya Nape akizungumza nje ya Ikulu akiwa na Rais Magufuli.

Kwa upande wa DC Mwegelo aliandika kwenye Instagram, “kuna anayebisha Rais Magufuli hashindi kwa asilimia 90 mwakani? Rais Magufuli uongozi anaujua in @harmonize_tz voice (kwa sauti ya Harmonize).

Nape aliomba msamaha kutokana na kusikika kwa sauti yake akizungumza na mtu anayeaminika kuwa ni Katibu Mkuu wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi, Abdullahman Kinana, ambapo mazungumzo yao yalikuwa na ukakasi dhidi ya Rais Magufuli.

Rais Magufuli alieleza kuwa baada ya kutafakari aliamua kumsamehe kwa kuzingatia jinsi alivyohangaika akiutafuta msamaha, ikiwa ni pamoja na kutuma jumbe za simu usiku wa manane na kuwaomba wazee wenye heshima nchini kumuombea msamaha.

Kabla ya kumsamehe Nape, Rais Magufuli alikuwa ameshawasamehe Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba na William Ngeleja kwa makosa kama yaliyokuwa yanamkabilia Nape.

Vincent Kompany aandaliwa mechi ya kuagwa
Wawekezaji kutoka Rwanda watua Kagera kuchangamkia fursa ya kilimo na ufugaji