Ujumbe wa Lady Jay Dee aliouweka kwenye mtandao wake wa Twitter mapema jana akijigamba kuwa hakuna kama yeye umehusishwa na tukio kubwa la kiungwana la Ruby kuiomba radhi Clouds FM na kurejeshwa rasmi kundini.
Jana, kipindi cha XXL kilifanikiwa kuteka anga la vipindi vya burudani baada ya kufanya mahojiano maalum na Ruby ambaye mwaka juzi alitangaza rasmi kuachana na uongozi wa Ruge Mutahaba ambaye ni Mkurugenzi wa Vipjindi na Uzalishaji wa kituo hicho, akitoa sababu za ‘maslahi’.
Kwa mujibu wa B12, Ruge alielekeza nyimbo za Ruby sisichezwe katika kituo hicho. Ruby hakuonekana kwenye Fiesta ya mwaka 2016 na 2017 kutokana na uamuzi huo.
Saa tatu baada ya kumalizika kwa kipindi hicho, Jide aliandika kupitia Twitter, “Huwa nikiulizwa nani anaweza kuja kuwa kama Mimi huwa sipati jibu. Nafikiri kwasababu kila mtu anaweza tu kuwa yeye kama yeye. Hakuna Komando kama Jide#Hakuna.
Huwa nikiulizwa nani anaweza kuja kuwa kama Mimi huwa sipati jibu. Nafikiri kwasababu kila mtu anaweza tu kuwa yeye kama yeye. Hakuna Komando kama Jide ?#Hakuna
— Lady JayDee (@JideJaydee) January 26, 2018
Baadhi ya mashabiki waliihusisha tweet hiyo na tukio hilo kutokana na historia ya uhasama kati ya Jide na uongozi wa kituo hicho uliodumu kwa miaka mingi, huku msanii huyo akigoma kuomba radhi kwa hiari hadi Mahakama ilipoamuru afanye hivyo baada ya kumkuta na hatia ya kutoa maneno yaliyogusa haki binafsi za Ruge na mmiliki wa kituo hicho, Joseph Kusaga. Unaweza kusoma ‘comments’ kwenye tweet ya hapo juu.
Jide alivaa majina ya ‘Binti Commando’, ‘Anaconda’ na mengine kutokana na misimamo yake na jinsi alivyoweza kusumbua kimuziki hata wakati wa uhasama huo.
Lady Jay Dee ni tunda la Clouds FM alipoanzia kama mtangazaji na baadaye kuwa mwanamuziki aliyesimamiwa na Ruge Mtahaba. Miaka michache baadaye, Jide aliingia kwenye mgogoro mkubwa na kituo hicho na nyimbo zake ziliamriwa kutopigwa rasmi tangu mwaka 2013 kabla ya kamba hiyo kulegezwa mwaka mmoja uliopita.
Hata hivyo, hakuna ushahidi wa moja kwa moja kama Jide alitupa jiwe gizani jana au vinginevyo.