Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais (Kazi, Uchumi na Uwekezaji) Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga ametoa rai ya kuendelea kuwawezesha na kuwajengea uwezo Walimu nchini, ili wawe wenye uwezo na ujuzi wa kutosha, hivyo kutoa elimu inayokusudiwa itakayoweza kuboresha rasilimali watu.
Soraga ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere wakati akihojiwa na kituo cha Televisheni cha Clouds kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Mtaji Rasilimali Watu.
Amesema, “ni kweli tunajenga miundombinu ya elimu, lakini tusisahau suala zima la kutoa mafunzo kwa Walimu wetu. Suala hili ni la msingi kwa sababu unaweza kuwa na miundombinu mizuri lakini kama hakuna Walimu bora, hizo juhudi zingine zote hazitokuwa na tija.”
Aidha, ameyataja mambo matatu ambayo amesema lazima yaangaliwe ili kuboresha elimu kuwa ni kuwekeza katika Walimu bora kwa kuwapa mafunzo na motisha za kutosha, kuangalia mitaala ya elimu kama inakwenda sambamba na uhalisia wa uchumi ambao nchi inakwenda nao na kutenga bajeti ya kutosha, kwa ajili ya uboreshaji wa elimu.