Ukarabati wa awamu ya kwanza unaoendelea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam, umefikia asilimia 95 na asilimia tano zilizobaki zinatarajiwa kukamilika ndani ya siku tano kuanzia jana Jumatatu (Oktoba 09).
Akikagua ukarabati huo uwanjani hapo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, amesema tayari vyumba vinne vya wachezaji vya kubadilishia nguo, sehemu ya kuchezea (Pitch), vyumba vya waamuzi, afya na eneo la video za marejeo (VAR) vimekamilika.
“Tayari taa za kisasa 320 za mfumo wa LED zimefungwa na kuna huduma ya mtandao wa bure kabisa wa ‘intaneti kwa ajili ya watazamaji wa mechi ambao tutauzindua kati ya tarehe 17 hadi 19, mwezi huu, kabla ya mchezo wa ufunguzi wa African Football League kati ya Simba SC na Al Alhy ya Misri Oktoba 20, mwaka huu,” amesema Ndumbaro.
Ameongeza kuwa, katika eneo la watu mashuhuri na sehemu ya waandishi wa habari kazi iliyobakia ni ndogo ambayo itamalizika ndani ya siku hizo tano akiongeza kuwa mfumo wa sauti uwanjani tayari umerekebishwa.
Dk. Ndumbaro amesema Kampuni ya Formula 360, itafunga mfumo wa matangazo kidijitali ambao utaanza kufanya kazi rasmi Oktoba 20, mwaka huu, huku akisisitiza kuwa baada ya mchezo huo, ukarabati mkubwa wa awamu ya pili utaendelea.