Ukarabati wa awamu ya kwanza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam umefikia asilimia 95 na zilizobaki zinatarajiwa kukamilika keshokutwa Jumamosi (Oktoba 14).
Akikagua ukarabati huo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema tayari vyumba vinne vya wachezaji, sehemu ya kuchezea, vyumba vya waamuzi, afya na eneo la video za marejeo (VAR) umekamilika.
“Tayari taa za kisasa 320 za mfumo wa LED zimefungwa na kuna huduma ya mtandao wa bure kabisa kwa ajili ya watazamaji wa mechi ambao tutauzindua kati ya Oktoba 17 hadi 19 kabla ya mchezo wa ufunguzi wa African Football League (AFL) kati ya Simba na Al Alhy ya Misri Oktoba 20,” amesema Ndumbaro
Ameongeza kuwa, katika eneo la watu mashuhuri na sehemu ya waandishi wa habari kazi iliyobakia ni ndogo ambayo itamalizika ndani ya siku mbili akiongeza kuwa mfumo wa sauti uwanjani tayari umerekebishwa.
Dk Ndumbaro amesema kuwa Kampuni ya Formula 360, imefunga mfumo wa matangazo kidijitali, ambao utaanza kufanya kazi rasmi Oktoba 20, huku akisisitiza kuwa baada ya mhezo huo, ukarabati mkubwa wa awamu ya pili utaendelea.