Ukarabati Uwanja wa Benjamin Mkapa, unaendelea kupamba moto baada ya serikali kuanza kwa kasi kutekeleza agizo la Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ na lile la Afrika ‘CAF’, kuelekea michuano ya African Football League ‘AFL’, ambayo ufunguzi wake utafanyika uwanjani hapo Oktoba 20, mwaka huu.
Michuano hiyo inayoshirikisha klabu nane bora barani Afrika, Simba SC ni timu pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki ‘CECAFA’, itakayoshiriki, ambapo pia itafungua kitimntim hicho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Al Ahly ya Misiri.
Akizungumza Uwanjani hapo, Meneja wa Uwanja huo, Paul Mahona, amesema wanakimbizana na muda kuhakikisha baadhi ya maeneo yamekamilika hadi ifikapo Oktoba 20, mwaka huu ili ufunguzi huo ufanyike uwanjani hapo kama ilivyopangwa.
Tunakimbizana na muda kuhakikisha siku chache zilizobaki tunazitumia vizuri ili ifikapo Oktoba 20, mwaka huu baadhi ya maeneo yawe yamekamilika ambapo Simba SC itaanza mchezo wake (dhidi ya Al Ahly),” amesema Mahona.
Meneja huyo amesema hadi kufikia tarehe hiyo, marekebisho ya awali yatakuwa yamekamilika na kwamba baadhi ya vitu vya zamani vilivyokuwa ndani ya uwanja huo tayari vimetolewa.
“Mkandarasi anaendelea kuyafanyia kazi maeneo hayo ikiwamo vyumba vya wachezaji tayari makabati yametolewa vilevile eneo la waandishi wa habari viti vilivyokuwapo vimetolewa, tunaamini uwanja huu utakuwa bora,” amesema meneja huyo.
Amesema maboresho hayo yatachukua muda mrefu kutokana kwamba kila eneo litaguswa na kuweka wazi kuwa wameimarisha usalama.