Wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, wametakiwa kuepukana na tabia ya umalizaji wa kesi za ukatili wa kijinsia kwa njia zisizofaa kwa kisingizio cha mila na desturi, na badala yake watumie sheria ili kukomesha matukio ya namna hiyo.
Wito huo umetolewa hii leo Oktoba 6, 2022 na Afisa Mradi wa Elimu ya Haki za Binadamu wa Shirika la Tusonge CDO, Consolata Kinabo kwenye Tamasha la Jinsia Kanda ya Kaskazini, Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
Amesema, “Tunakwepa kufuata sheria na tunamaliza kesi za ukatili wa kijinsia kienyeji kwa visingizio vya mila na desturi zetu na matokeo yake wahanga wanazidi kuathirika na yanakuwa ni mazoea katika jamii kwa sababu wanaona hakuna sheria yoyote inayochukuliwa kwa wanaofanya ukatili.”
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa warsha hiyo, Sauda Mshana amesema siyo kila tukio la ukatili wa kijinsia linatokana na mila na desturi kandamizi, bali wakati mwingine hutokana na tabia binafsi ya muhusika wa tukio.