CCM na Ukawa wameingia katika mvutano mwingine baada ya pande zote kutaka kurusha matangazo ya moja kwa moja kwenye TV Jumamosi hii kila upande ukitaka kuonesha mkutano wa mgombea wao wa urais.

Wakati chama Chadema na Ukawa wakitaka kurusha moja kwa moja mkutano wa uzinduzi wa kampeni zao kutoka Dar es Salaam Jumamosi hii, CCM pia wamepanga kurusha moja kwa moja mkutano wa mgombea urais wao utakaofanyika jijini Mbeya, muda uleule.

Katibu  wa Itikadi na Uenezi  wa CCM, Nape Nnauye amesema kuwa chama hicho tayari kimeshalipia vituo kadhaa vya televisheni nchini kwa ajili ya kuonesha moja kwa moja mkutano wa Dk. Magufuli siku ya Jumamosi kutoka Mbeya.

“Ni kweli mgombea wetu akiwa Mbeya tutarusha matangazo ya kampeni zake moja kwa moja kwenye runinga, sasa ni vituo vingapi vya runinga siwezi kujua maana kuna watu wanalifanyia kazi suala hilo,” Nape alikaririwa na gazeti la Mwananchi.

Alieleza kuwa kama Chadema wangefahamu kuwa wanataka kuonesha mikutano yao moja kwa moja wangewahi mapema.

Chanzo kimoja kutoka kwenye kililiambia gazeti hilo kuwa CCM na Chadema waliomba nafasi ya kurusha matangazo kwenye kituo chake (Jina halikutajwa) lakini CCM ndio waliopewa na fasi.

Naibu Mkurugenzi wa Azam TV, Tido Mhando aieleza kuwa endapo vyama hivyo viwili vitahitaji kulipia kupata huduma hiyo vitapewa kwa kuwa kila chama kitaoneshwa kupitia channel tofauti kwa kuwa kituo chake kina channel tofauti.

Ukawa wamepanga kuzindua rasmi kampeni zao Jumamosi, Agosti 29 mwaka huu.

 

"Dk. Slaa Kujiunga Na Uzinduzi Wa Ukawa Jangwani"
Udhamini Wazidi Kumiminika Soka La Bongo