Wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana walitoka Bungeni baada ya kiongozi wa Kambi ya upinzani, Freeman Mbowe kutoa hoja tatu za kupinga muenendo wa Serikali na Bunge.

Mbowe aligoma kuwasilisha maoni ya kambi ya upinzani kuhusu makaridio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2016/17 na badala yake alitoa hoja tatu huku akiungwa mkono kwa shangwe za wabunge wa upinzani.

Katika hoja yake ya kwanza, Mbowe alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikiongoza bila kuwa na muongozo halali wa kisheria kama inavyotaka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kuwa Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mawaziri ya Mwaka 1980, kifungu cha 5(1) inamtaka Rais kila anapounda Baraza la Mawaziri kuchapisha kwenye gazeti la Serikali Muundo wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali yake. Alisema kuwa jambo hilo halijafanywa na serikali ya Awamu ya Tano jambo linalopelekea kuongoza kwa kauli mbalimbali za rais na mawaziri bila kufuata muongozo wa kisheria.

Katika hoja yake ya pili, Mbowe alieleza kuwa Serikali imekwapua uhuru wa Bunge  huku akipinga vikali kitendo cha Ofisi ya Bunge kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia Shirika la Habari la Taifa (TBC) na hata kwa vyombo binafsi.

Alisema kuwa kitendo hicho ni uvunjifu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoeleza kuwa kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake na kueleza fikra zake; ana haki ya kupata habari na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi na kwamba ana haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake. Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kwa maisha na shughuli muhimu na masuala muhimu kwa jamii.

“Bunge ni chombo cha wawakilishi wa wananchi na wananchi wana haki ya kujua Bunge lao linavyofanya kazi ili wawe na uwezo wa kuwawajibisha wawakilishi wao iwapo hawafanyi kazi ianvyostahili. Katika hali isiyo ya kawaida, Serikali imepokonya wananchi haki ya kupata habari za Bunge kwa kuzuia mijadala ya Bunge isioneshwe moja kwa moja na Televisheni ya Taifa [TBC1] na vyombo vingine binafsi,” alisema Mbowe.

Katika hoja ya tatu, Mbowe alieleza kuwa Serikali imekuwa ikiingilia majukumu ya Bunge na kufanya maamuzi yaliyopaswa kufanywa na muhimili huo. Alieleza kuwa Serikali imekuwa ikivunja Katiba na Sheria kwa kufanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge.

Alisema Ibara ya 63(3) (b) inalipa Bunge mamlaka ya kujadili na kuidhinisha Bajeti ya serikali. Pia, aliitaja Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2000 inayoitaka Serikali kuwasilisha Bungeni bajeti ya nyongeza ili kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha zilizoidhinishwa awali hazikutosha.

Mbowe alieleza kuwa endapo hayo hayatafanyiwa kazi, wanaendelea kutafakari kuhusu ushiriki wao kwenye mjadala wa bajeti.

Akizungumza baada ya Mbowe na wabunge wa Ukawa kutoka nje ya Bunge, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alieleza kuwa madai yao ni mazito kwakuwa wanadai kuvunjwa kwa Katiba ya nchi, hivyo walipaswa kufuata taratibu za kisheria [ikiwa ni pamoja na kwenda mahakamani].

Ofisi ya Waziri Mkuu kutumia Bodaboda, Bajaji kubana matumizi
Yanga yarejea kutoka Misri, Mashabiki waipoza ‘Airport’