Wakati juhudi zinazofanywa na wanaharakati wa kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukeketaji na kupinga mila hiyo hapa nchini zikiendelea, baadhi ya jamii zinazo jihusisha na ukeketaji zimeanza kuwageukia watoto wachanga.
Hayo yamebainishwa na program meneja wa shirika lisilo la kiserikali la mtandao wa kudhibiti ukeketeji (NAFGEM) Honoratha Nasua, alipokuwa anazungumza wakati wa maonesho ya wiki ya AZAKI.
Nasua alibainisha kuwa takwimu za matukio ya ukeketaji zimebadilika na kuonesha jamii imeanza kuwakeketa watoto wachanga, tofauti na awali ambapo walikuwa wanawakeketa walio na umri kati ya miaka 14 hadi 20.
Jambo linalopelekea ukwamishwaji wa juhudi za kukomesha ukeketaji kwasababu watoto wachanga hawawezi kujitetea kama wale wakubwa ambao wakipata elimu wanaweza kujitetea wenyewe hata kwa kutoroka.
Aidha shirika la NAFGEM limeahidi kuwa litaendelea kufanya kazi za kuelimisha jamii kuachana na mila za ukeketaji, mimba za utotoni na kuwasaidia kupata elimu wale wanaotoroka mila hizo katika mikoa ya Kilimanjaro na Manyara.