Watu wanne wilayani Ukerewe, Mkoani Mwanza wamefariki huku wengine 27 wakijeruhiwa baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria katika Ziwa Victoria kupigwa na radi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Muliro Jumanne amesema, tukio hilo limetokea Juni 23 mwaka huu saa 2:45 asubuhi katika Kitongoji cha Busele, Kata ya Bubiko, wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.
Muliro amesema, mtumbwi huo wa abiria unaojulikana kama One Ten wenye namba za usajili 00238 unaofanya safari za Kome na Bugaza ulipigwa radi na kusababisha vifo vya watu wanne pamoja na majeruhi 27 ambapo kati yao ni wanawake 12 na wanaumme 15.
Alitaja majina ya waliofariki kuwa ni ;
1. Deogratus mulungu, (50), mkara.
2. Kumunya andrea, (36), mkerewe,
Ambaye alikuwa ni nahodha wa mtumbwi.
3. Simon cherles, (36), msukuma,
Aliyekuwa nahodha msaidizi.
4. Ndege abdu, (25), mjita.
Amesema Miili ya marehemu wote imefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Pia amesema, majeruhi wamefikishwa katika Zahanati ya Kijiji cha Bukiko na wengine Kituo cha Afya cha Bwisya kwa ajili ya matibabu, huku baadhi wametibiwa na kuruhusiwa.