Mkurugenzi wa kuratibu na kukuza utafiti kutoka Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) Dkt. Paul Kazyoba, amesema kilevi cha aina yoyote hakitakiwi kwa masaa 72 baada ya kupata chanjo kwani kitaingilia mfumo wa uzalishaji wa kinga za mwili ambao unafanywa na chanjo kwa saa za mwanzo.

Dkt Kazobya amesema kuwa kutokupata kilevi cha aina yoyote ile kwa masaa hayo ambayo ni kama siku tatu ni zingatio muhimu watu wanatakiwa kulifuata.

Aidha Wataalamu wa afya na watafiti wa chanjo wanasema pombe na dawa ya chanjo vyote vinakwenda kwenye ini, hivyo upo uwezekano wa ini kuongezewa mzigo na kulichosha lakini pia kilevi huingilia kazi ya dawa kama ilivyo kwa dawa zingine hivyo kupunguza ufanisi.

Dkt. Kazyoba amesema chanjo inapochomwa katika mwili wa binadamu, ikiingia inaenda kuzisisimua seli za kinga ‘antibodies’  zinazalishwa zikishajaa mwilini zinakua askari wa kupambana na kirusi kitakachoingia.

“Kuufanya mwili uzalishe hizi seli kinga, inatakiwa usiingiliwe na kitu chochote cha tofauti kwenye damu kwa saa 72. Kilevi cha aina yoyote kwa maana ya pombe, bangi, shisha au dawa za kulevya lazima kitaingilia mfumo na hivyo kuifanya chanjo kutofanya kazi yake vizuri.

“Ndani ya saa 72 ni muda ambao kazi kubwa inafanyika hapo na ndiyo maana maudhi madogo madogo mtu anayapata ndani ya huo muda, vilevi vitaathiri uzalishaji wa mwanzo wa seli za kinga, ambazo zitajitengeneza mwilini mwako kwa miezi kadhaa,” Amesema Dkt Kazyoba.

Hali kadhalika Dkt Kazobya ameainisha jambo lingine muhmu la kuzingati wakati wa chanjo ni kuhakikisha mwili uko sawa na wenye nguvu za kutosha.

“Muda huo unaingiza kitu kipya mwilini, unaposhtuka na kuanza kupata uchovu na maudhi pale ndiyo unazalisha seli kinga  kuuandaa mwili ili adui akijaribu kuingia akutane na kinga muda huo kama ukiona maudhi yanazidi mtafute daktari japokuwa wanaopata hali hiyo ni wachache,” Amesema Dkt Kazobya.

Hata hivyo mambo ya kuzingatia baada ya kuchoma chanjo, inatakiwa mtu aushughulishe mwili kwa kipindi cha saa 72 za awali kwani kwa kufanya hivyo seli za kinga huzalishwa kwa wingi na huwa na manufaa zaidi tofauti na kinyume chake.

TANESCO yasisitiza utunzaji wa miundombinu
Waziri Kabudi ahimiza ujenzi wa Mahakama Manyoni