Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, amesema baadhi ya viongozi wamekuwa wanashindwa kuibana Serikali katika mambo ya msingi kwa kuhofia kupoteza nafasi zao, huku wakisahau kwamba kitendo cha kusifia kila kitu na ukimya wao unawaumiza Wananchi, na hivyo kuwataka waache unafiki.
Msambatavangu ameyabainisha hayo wakati akiongea na Dar24 Media na kuongeza kuwa maendeleo yoyote huja kwa ushirikiano na ni lazima awepo kiongozi ambaye atawakilisha wengine, hivyo wanapoaminiwa na kushindwa kuzitumia nafasi hizo kiufasaha ni kusababisha adha kwa waliomuamini huku akisema hiyo ni dhana ya ‘Uchawa’ (kujipendekeza kwa lengo fulani).
Amesema, Kiongozi yeyote anayetambua majukumu yake huwa ni mfuatiliaji wa mambo na hutoa kauli zinazotosha kukupa picha ya moja kwa moja ya wapi mnaelekea katika utekelezaji wa mambo au shughuli za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo huku akipewa wadhifa wa ubeba maono na kujivunia uwepo wake.
“Lakini ili kufanikisha mambo pia ni lazima uwepo ushirikiano baina yake na waongozwaji (Wananchi) ambao nao wanatakiwa kufahamu kwamba kabla ya kutaka kufanyiwa mambo makubwa na yenye thamani watakayoyafurahia katika maisha, ni lazima wajiulize thamani yao katika kutenda kwa wengine yale wanayoyapenda. tuwajibike,” alisema Msambatavangu.
Mbunge huyo ameongeza kuwa, “watu wanawaza kujipendekeza lakini hawana ujasiri wa kutengenezea mafanikio kwa jitihada binafsi “self made” Siku hizi uchawa umekuwa ni kama taaluma na kuna watu na elimu zao na kazi zao lakini wanaona kusifia, kupongeza na kuudhalilisha utu wao ni jambo la kawaida na hawajali hata kama ni kwa mambo yasiyo na lakini msimamo wao ni kusifia na kupongeza huku wakiona kujiita chawa ni jambo la sifa na la kujivunia.