Lydia Molell – Morogoro.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua ripoti ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI ambayo inaonesha maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Desemba mosi, 2023 katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Morogoro, mjini Morogoro na kudai kuwa Serikali iliamua kufanya utafiti kwa lengo la kujua hali ya sasa ya VVU na UKIMWI ilivyo hapa nchini na matokeo yameonesha kuna makubwa.
Amesema, “maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua kutoka watu 72,000 waliokuwepo mwaka 2016/2017 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022/2023. Hii ni sawa upungufu wa asilimia 0.18 ambapo asilimia 0.24 ni wanawake na asilimia 0.11 ni wanaume.”
Utafiti huo, unaotambulika kama Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI kwa mwaka 2022/2023 unapima matokeo ya mwitikio wa kitaifa wa UKIMWI nchini miongoni mwa watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15 ukiwa na lengo la kukadiria kiwango cha maambukizi mapya ya VVU, ushamiri wa VVU, ufubazaji wa VVU kwa watu wanaoishi na VVU na utumiaji wa dawa kitaifa na kimikoa.
“Utafiti umebaini kuwa kiwango cha kufubaza VVU kimeendelea kukua ambapo kwa sasa ni wastani wa asilimia 78 ambapo kwa upande wa wanawake kiwango kimekua kwa asilimia 80.9 na wanaume asilimia 72.2 ikilinganishwa na asilimia 52 iliyokuwepo kulingana na utafiti wa mwaka 2016/2017,” ameongeza Majaliwa.
Kuhusu kiwango cha ushamiri wa VVU kwa umri kuanzia miaka 15 na zaidi kwa mikoa ya Tanzania bara, Waziri Mkuu amesema utafiti umeonesha kuwa, kinaanzia asilimia 1.7 kwa mkoa wa Kigoma hadi kufikia asilimia 12.7 kwa mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa.
“Mkoa wa Njombe una viwango vya ushamiri zaidi ya asilimia 9 sawa na mara mbili ya kiwango cha Taifa. Kwa upande wa Zanzibar, yanaonesha unaanzia asilimia 0.2 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba hadi asilimia 0.8 Mkoa wa Kusini Unguja,” amesema.