Tabia ya ukimya ambao haukuzoeleka kuonekana kwa Mbunge wa Kibamba na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika imeibua wasiwasi na tetesi kuwa huenda hayuko pamoja na chama chake hicho na kwamba anapinga uwepo wa Edward Lowassa aliyepewa nafasi ya kugombea urais kupitia chama hicho.

Ukimya huo ulioacha maswali umeendelea kuwachanganya wananchi hasa baada ya kusambazwa waraka wenye jina la mbunge huyo ukiwa na maelezo mazito akionesha kukipinga chama chama chake kwa kumpokea na kumpa nafasi Lowassa.

Mnyika na Lowassa

Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana la Chadema, Edward Simbeye leo amekanusha vikali taarifa hizo na kueleza kuwa waraka huo unayosambazwa hauna uhusiano wowote na Mnyika. Aliwarushia lawama CCM kwa kile alichodai wanapika propaganda hiyo.

Simbeye amelitaka Jeshi la polisi kushirikiana na TCRA ili kumbaini na kumtia nguvuni mtu aliyehusika kuandaa barua hiyo na kuisambaza mitandaoni.

“Hoja hiyo ni ya kupuuzwa kwa kuwa haina ukweli wowote ule, na nitalishangaa Jeshi la Polisi kuendelea kukaa kimya,na kumuacha aliepotosha Umma kwa kiwango kikubwa kiasi hicho,jambo ambalo limempa Usumbufu mkubwa Naibu Katibu mkuu kwa chama na Wananchi wake katika jimbo lake,” amesema Simbeye.

Hata hivyo, Simbeye hakujibu swali linalopelekea kuwepo kwa sintofahamu hiyo, kuhusu sababu za ukimya wa mwanasiasa huyo machachari.

UVCCM waionya BAVICHA, wadai watapambana kama ‘MauMau’
Lowassa ateta na Rais Kenyatta, Rutto nchini Kenya