Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amepiga marufuku uuzwaji wa fomu za uchaguzi ambazo walikuwa wakiuziwa wagombea kwaajili ya kugombea katika nafasi mbalimbali katika ngazi za Wilaya, Mkoa na taifa.
Aidha, katika taarifa iliyotolewa na CCM Makao Makuu imesema kuwa, jambo hilo halijawahi kupata ridhaa ya kikao chochote cha chama, kwani ni kinyume cha katiba na kanuni za uchaguzi wa CCM.
“Jambo hili kama likiachwa linaweza kuleta madhara makubwa katika chama chetu, kwani litawagawa wanachama kwa uwezo wao wa kipato na kujenga matabaka miongoni mwao,”imesema taarifa hiyo.
Hata hivyo, amesema kuwa ili kuepuka matabaka ya walionacho na wasionacho ndani ya chama, Katibu Mkuu amepiga marufuku uuzwaji wa fomu hizo kwakuwa hakuna kikao chochote kilichobariki kufanya hivyo.