Mshambuliaji anayeongoza kwa upachikaji wa mabao kwenye timu ya taifa ya England kwa wakati wote, Wayne Mark Rooney ataendelea kuwa anahodha wa timu hiyo chini ya utawala mpya wa kocha Sam Allardyce.

Rooney ambaye ameshaifungia England mabao 53 katika michezo 116 aliyocheza tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza katika timu ya taifa ya wakubwa mwaka 2003, ameteuliwa na kocha huyo kuendelea kuwa nahodha.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, alianza kuonyesha hofu ya kupokonywa madaraka ya unahodha siku chache baada ya chama cha soka nchini England FA kumtangaza Allardyce kama mrithi wa Roy Hodgson, ambaye alijiuzulu kufuatia kushindwa mtihani wa kufanya vyema wakati wa fainali za Euro 2016.

Allardyce alitangaza kikosi chake kwa mara ya kwanza mwishoni mwa juma lililopita tayari kwa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 dhidi ya Slovakia, lakini hakuainisha ni nani angekua nahodha.

Akiwa katika mkutano na waandishi wa habari hapo jana, kocha huyo ambaye aliwahi kuwa meneja wa baadhi ya klabu za ligi kuu ya nchini England, alisema Rooney bado anastahili kuendelea na jukumu la kuwaongoza wachezaji wenzake uwanjani.

Alisema anatambua umuhimu wa mshambuliaji huyo kuendelea na cheo chake na hatokua na maamuzi mengine kwa sasa mpaka hapo baadae atakapoamua mambo mengine.

Image result for Wayne Rooney to remain England captain under Sam Allardyce.Kocha wa timu ya taifa ya England Sam Allardyce.

“Wayne amekua kiongozi mzuri kwa timu ya taifa ya England, kutokana na tabia yake na wakati mwingine huchukua jukumu la kuwatuliza wachezaji wengine pale linapotokea tatizo,”

“Rekodi ya Wayne inajieleza yenyewe na ninaamini klila shabiki wa soka atakubaliana na mimi. Amekua mchezaji mwenye historia ya kipekee katika kikosi cha England cha sasa, kutokana na ukongwe alionao tofauti na wengine niliowaita.

“Kwa sababu hizo sina budi kuendelea kumpa heshima yake ya kuwa kiongozi wa wenzake uwanjani na ninaamini ataendelea kufanya makubwa zaidi kwa kunisaidia mimi pamoja na viongozi wengine katika benchi la ufundi.” Alisema Allardyce

Rooney anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari hii leo huko St George’s Park kwa ajili ya kutoa maelezo ya kina kuhusu heshima ya unahodha ambayo anaendelea kuwa nayo, pamoja na matarajio yao kuelekea katika mchezo wa dhidi ya Slovakia ambao umepangwa kuchezwa mjini Trnava, mwishoni mwa juma hili.

Hamisi Kiiza Amfuata Mrisho Ngassa Afrika Kusini
GK aukacha muziki wa Rap