Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema sekta ya viwanda ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini nchini, pamoja na kuboresha maisha ya Watanzania.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo mkoani Kilimanjaro baada ya kuzindua upanuzi wa kiwanda cha bia cha Serengeti tawi la Moshi akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.
“Duniani kote, sekta hii imekuwa chimbuko la maendeleo ya haraka na ndiyo mhimili mkuu wa kutegemewa katika kuongeza thamani ya malighafi, kutoa ajira kwa wananchi, kuongeza mapato ya Serikali pamoja na fedha za kigeni, kuongeza na kuboresha teknolojia,” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema kwa kulitambua hilo, Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda kwa kuboresha miundombinu muhimu na wezeshi kama reli ya Uhuru, ujenzi wa reli ya kisasa ili ziweze kubeba mizigo mizito na kuisafirisha kwa haraka kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Aidha Majaliwa ametoa wito kwa Wawekezaji na wazalishaji kuchangia katika juhudi zinazofanywa na Serikali kuondoa changamoto zinazoathiri ukuaji wa sekta ya viwanda kwa kuzalisha bidhaa nyingi zenye ubora wa juu na kwa bei shindani ambayo hata mlaji wa kawaida atamudu kununua bidhaa hizo.