Miongoni wa wabunge waliowasilisha maombi ya kugawa majimbo yao ili kuwa mawili kutokana na ukubwa na wingi wa watu ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ni.
Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 3, 2023 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Ummy Nderiananga wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda.
Katika swali lake Mwakagenda aliuliza ni lini serikali italigawa jimbo la Mbeya mjini kutokana na ukubwa wake ambapo Naibu Waziri Ummy alisema, “Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye ni Spika wetu Tulia ameshawasilisha suala hili muda utakapofika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi italitizama Jimbo la Mbeya Mjini.”
Naye Mbunge wa Kilindi Omari Kigua aliuliza ni lini Serikali italigawa Jimbo la Kilindi kutokana na jiografia yake ambapo Naibu Waziri alisema kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ipo katika maandalizi mbalimbali ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
“Kwa kuzingatia taratibu na vigezo, muda wa kugawa majimbo utakapofika Tume itatoa tangazo rasmi kwa wadau wote wa uchaguzi juu ya kuanza kwa machakato wa ugawaji wa majimbo ili wadau wawasilishe maoni na maombi yao na hivyo kushughulikiwa kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa kikatiba,”amesema.