Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Jestus Nyamanga, amekanusha taarifa zinazoenea mitandaoni kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya limeifutia misaada Tanzania na kwamba linapanga kuiwekea Tanzania vikwazo vya kiuchumi.

Akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa na Ubalozi huo, Balozi Nyamanga ambaye pia ni mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya, amesema kuwa kilichotokea ni kuwa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Ulaya ilikaa kikao chake cha kawaida na kujadili masuala kadhaa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa miongoni mwa masuala ambayo yalijadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na hali ya amani nchini Tanzania baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu, jambo ambalo ni utaratibu wa kawaida wa kamati hiyo kuweka majadiliano na nchi ambazo ni ubia wao mkubwa wa maendeleo pindi uchaguzi unapokamilika katika nchi hiyo.

Balozi Nyamanga amesema taarifa zinazoenea kuwa Bunge lote la Umoja wa Ulaya limeazimia kusitisha misaada kwa Tanzania na mikopo kutoka Umoja wa Ulaya na mashirika yake na kwamba Bunge hilo limeazimia kuiwekea Tanzania vikwazo ni za upotoshaji na hazina ukweli wowote.

Aidha Balozi Nyamanga amekanusha pia taarifa kuwa Bunge hilo limeazimia kuizuia Tanzania, kuuza bidhaa zake katika nchi za Umoja wa Ulaya akisema “taarifa hizo ni za uwongo mtupu, hazina ukweli wowote na ni za kupotosha,”

Balozi Nyamanga amefafanua kuwa kikao kilichokaa Novemba 19 ni cha Kamati ya Bunge na si kikao cha Bunge lote la Umoja wa Ulaya na kusisitiza kuwa hata kikao hicho cha kamati ya Bunge hakikutoa azimio lolote kuhusu Tanzania.

“Kilichofanyika ni kuwapa wabunge kujadili kutoa mawazo yao kuhusu hali ya Tanzania baada ya Uchaguzi, na ni wabunge watano tu waliotoa mawazo yao kati ya wabunge 71 wa kamati hiyo, Bunge lote la Umoja wa Ulaya lina jumla ya wabunge 705,” amesema Balozi Nyamanga.

Bofya link hapa chini …

Maalim Seif ajibu baada ya kupokea barua ya Rais Mwinyi
BOT yachukua usimamizi China Commercial Bank