Njegere ni mboga yenye virutubisho vingi vinavyofanya kazi ya kujenga mwili, kuboresha ufanyaji kazi wa ini na ni chanzo kizuri cha Protini.
Ulaji wa njegere mara kwa mara husaidia kuboresha kinga ya mwili, hurekebisha kiwango cha sukari kwenye damu lakini pia huzuia mtu kuzeeka kwa haraka na zina kiwango kidogo cha kalori.
Njegere zina kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi, vitamin A,B, na C na hazina mafuta yanayoweza kuganda katika mishipa ya damu.
Ulaji wa njegere za kijani huongeza damu, hukabiliana na udhaifu wa afya lakini zinasaidia kupunguza maumivu katika kidonda kinachouma kwa sababu inasaidia kuondoa asid zilizopo tumboni.
Kwa mujibu wa Mtaalamu wa tiba-lishe wa taasisi moja nchini Marekani, Dk.George Mateljan anasema, njegere ni miongoni mwa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha kamba lishe zenye uwezo wa kushusha kiwango cha lehemu inayosababisha shambulio la moyo.
Matokeo ya utafiti wake huo aliouandikia kitabu kiitwacho The World’s Healthiest Foods, asilimia 65 ya mbegu ya njegere ni kamba lishe ambapo pamoja na kushusha lehemu, pia huondoa shinikizo ya damu na kuzuia shambulio la moyo.