Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amelitaka Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kujipanga kibiashara pamoja na kiubia na makampuni binafsi ya uwekezaji mara baada ya kufufuliwa na kuzinduliwa rasmi ili liwe na tija kwa wavuvi na taifa kwa ujumla.
Naibu Waziri Ulega amesema hayo mara baada ya kufika katika ofisi za TAFICO zilizopo Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam na kufafanua kuwa ni lazima uwepo mkakati na mbinu za kujielekeza zaidi katika uchumi wa bluu ili nchi ifaidike rasilimali samaki na mazao yake lakini pia kuhakikisha uchumi wa wavuvi wadogo unakua ili shirika hilo liwe na tija zaidi.
Aidha Ulega amemuelekeza Mwenyekiti wa Bodi ya TAFICO Prof. Yunus Mgaya kusimamia mbinu na mkakati imara wa ufufuaji wa shirika na kumpongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
“Hivi karibuni haitazidi miezi mitatu tunapokea meli ya uvuvi tunataka ikifika ianze kazi mara moja, meli ikute tumekaa kwenye mpango kazi iende kuvua samaki wa kutosha bahari kuu na ilete hao samaki kwa wingi wauzwe ndani na nje ya nchi.” Amefafanua Mhe. Ulega
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa TAFICO Esther Mndeme amesema ukarabati unaendelea kufanywa katika miundombinu mbalimbali iliyopo kwenye eneo hilo baada ya serikali kufufua shirika hilo na kwamba baadhi ya miundombinu inahitaji ukarabati mkubwa kutokana na miundombinu hiyo kutofanya kazi kwa takriban miaka ishirini.
Meneja wa TAFICO Mndeme amesema licha ya changamoto za kifedha Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ukarabati huo unafanyika kwa muda uliopangwa ili shirika lianze majukumu yake rasmi kama ambavyo imekusudiwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAFICO Profesa. Yunus Mgaya, amesema shirika likianza kufanya kazi vizuri litaleta tija katika uchumi wa bluu kwa kuwa fursa nyingi zitafunguka na taifa kupata tija zaidi kiuchumi na wavuvi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa amesema uwepo wa TAFICO katika wilaya hiyo kutaongeza chachu ya maendeleo kwa wakazi wa wilaya hiyo kwa upande wa ajira pamoja na kuhakikisha sekta ya uvuvi inakua.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amefanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Dar es Salaam kwa kujionea utendaji kazi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na ukarabati wa majengo ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).