Ulinzi mkali wa vikosi vya kutuliza ghasia umeshuhudiwa kwenye jiji la Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wakati matokeo ya uchaguzi wa urais yakitarajiwa kutangazwa muda wowote.
Viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na wafuasi wao wameonesha wasiwasi wao kuwa ulinzi unaoonekana katika maeneo mbalimbali huenda ukawa unaashiria kuwa matokeo yatakayotangazwa yanaweza kuwa tofauti na yanavyotarajiwa na wananchi wengi.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) jana ilieleza kuwa bado haijakamilisha zoezi la kuhesabu na kujumlisha kura za baadhi ya vituo na kwamba inafanya pia mikutano kadhaa ya tathmini.
Wakati hayo yakiendelea, majirani zao, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na Rais wa Zambia, Edgar Lungu kwa pamoja wameitaka CENI kutangaza matokeo ya uchaguzi huo haraka iwezekanavyo kwani kuchelewa kunaweza kuondoa imani ya wananchi.
Viongozi hao waliofanya mkutano wa dharura jijini Pretoria ambapo baada ya mkutano wao, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini alieleza kwa ufupi walichojadiliana.
“Maraisi hawa wawili wameitaka CENI kuharakisha kukamilisha zoezi la kuhesabu na kujumlisha kura pamoja na kutangaza matokeo ya uchaguzi ili kuhakikisha wanatunza imani yake kwa wananchi,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje.
“Viongozi hawa wametahadharisha kuwa kuchelewa kutangaza matokeo ya uchaguzi kunaweza kusababisha kutoweka kwa imani na kuharibu amani na utulivu wa nchi,” aliongeza.
CENI imetaja sababu za kuchelewa kuwasilishwa kwa taarifa kutoka kwenye vituo mbalimbali vya kupigia kura kuwa ndio chanzo cha kuchelewa huko. Jana, iliahidi kutangaza matokeo hayo baada ya saa 24 au saa 48.