Kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Uongozi wa Young Africans umeongeza ulinzi katika kambi ya kikosi cha klabu hiyo Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Young Africans inatarajiwa kuikaribisha USM Alger ya Algeria katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa fainali utakaopigwa Jumapili (Mei 28) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kabla ya kurudiana Juni 3, mjini Algiers.
Katika mchezo huo Young Africans wanahitaji ushindi wa mabao zaidi ya matatu ili wawape ugumu wapinzani wao watakapokuwepo nyumbani katika mchezo wa marudiano.
Inaelezwa kuwa kambini huko haitajiki kiongozi yeyote zaidi ya wachezaji na benchi la ufundi pekee ili kuongeza utulivu.
Mtoa taarifa hizi amesema kuwa kikosi hicho mara baada ya juzi Jumatatu (Mei 22) kurejea jijini Dar es salaam, wakitokea mkoani Dodoma kwa ndege moja kwa moja kiliingia kambini tofauti na awali walikuwa wakipewa mapumziko ya siku moja hadi mbili kwa ajili ya kwenda kusalimia familia zao.
Ameongeza kuwa hakuna mchezaji yeyote aliyepewa ruhusa ya kurejea nyumbani kwake, lengo kocha Nasreddine Nabi apate muda wa kuwapa mbinu za kiufundi zitakazowawezesha kutwaa taji hilo.
“Katika kuelekea michezo hiyo miwili, tunafahamu kabisa wapo baadhi ya viongozi wa tu na Serikali watataka kwenda kambini kwa ajili ya kuzungumza na wachezaji kwa lengo la kuwapa hamasa.
“Hivyo hatutaki hilo litokee, na badala yake tumezuia watu kwenda kambini kwa lengo la kumpa utulizu kocha wa kukiandaa kikosi chake kwa siku hizi tano.
“Kitendo cha viongozi kwenda kambini kila wakati kutawavuruga wachezaji na badala ya kucheza kwa presha kubwa katika michezo hii miwili ya fainali,” amesema mtoa taarifa hizi