Kulingana na maoni ya Wananchi, wanasema Chama tawala Afrika Kusini cha African National Congress – ANC, kilichopo madarakani tangu mwaka 1994, kimepungukiwa na Wanachama hadi chini ya asilimia 50 ikiwa ni kipindi kifupi kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika hapo mwakani 2023.
Kwa mujibu wa kura ya maoni ya Taasisi ya Utafiti wa Jamii – SRF, Chama hicho, kilichowahi kuongozwa na Baba wa Taifa hilo, Hayati Nelson Mandela huenda kikapata asilimia 45 ya kura mwakani, dhidi ya asilimia 31 ya chama cha Democratic Alliance – DA.
“Takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha wanaokiunga mkono chama cha ANC kinaonekana kupungua kwa kiasi fulani,” ilisema ripoti hiyo ya SRF. Uungwaji mkono kwa ANC umepungua kutoka asilimia 52 mwezi Machi kulingana na kura ya maoni, ambazo zinatokana na mahojiano na wawakilishi zaidi ya 1,400 waliojiandikisha kijiografia na kidemografia Oktoba,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, wataalamu wa Takwimu hizo wanasema endapo uchaguzi ungefanyika kesho, chama cha tatu kwa ukubwa Afrika Kusini, cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters – EFF, kingepata asilimia tisa ya upendeleo, ambapo ANC haijawahi kupata chini ya asilimia 50 ya kura katika uchaguzi wa kitaifa tangu kurejea kwa demokrasia miongo mitatu iliyopita.