Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kumpa maelezo ndani ya siku saba kuhusu chanzo cha kukatika umeme mara kadhaa katika sehemu kubwa ya nchi.
Akizungumza leo jijini Dodoma na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo mbele ya waandishi wa habari, Dkt. Kalemani ameitaka Bodi hiyo kufanya uchunguzi mahususi wa tatizo hilo kwa kuhusisha vyombo vingine vyenye uwezo wa kusaidia upatikanaji wa majibu husika ili tatizo hilo lisijirudie.
Aidha, Dkt. Kalemani amesema kuwa kwakuwa tatizo hilo linapotokea linaweza kusababishwa na uzembe pamoja na hujuma, ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha inawaondoa naibu mkurugenzi wa uzalishaji na naibu mkurugenzi wa usambazaji.
“Jambo hili linapotokea maana yake kuna uzembe katika usimamizi, ama kuna kutokufuatilia maelekezo ya Serikali au kunaweza kukawa na hujumu kwa baadhi ya watumishi wasio wazalendo; kwahiyo kuanzia sasa Bodi ichukue hatua dhidi ya Naibu Mkurugenzi wa Generation (Uzalishaji), Naibu Mkurugenzi wa Transmission (usambazaji). Ichukue hatua za kiutawala ikiwa ni pamoja na kuwavua nyadhifa zao kuanzia leo,” alisema.
Amefafanua kuwa nchi inapokuwa gizani ndani ya nusu saa tu maana yake usalama unakuwa hatarini pamoja na kusimama kwa uzalishaji katika viwanda, hivyo Serikali inakosa mapato.
Aidha, ameagiza Tanesco kuhakikisha kuwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu iunganishe umeme katika maeneo yote ya mijini ambayo tayari yapo kwenye mpango wa Shirika hilo.
“Yapo maeneo ya mijini ambayo yanahitaji kuunganishiwa umeme na yamekaa bila umeme muda mrefu na huku yako ndani ya mipango ya Shirika, na pesa mmeshatoa kila mkoa. Kwahiyo, Serikali inataka kuona maeneo hayo yanafikishiwa umeme ndani ya miezi mitatu,” alisema.
Pia, aliagiza wateja wote nchini ambao tayari wameshalipia bili zao kuunganishiwa kabla ya Disemba 31 mwaka huu.
Kadhalika, alilitaka Shirika hilo kuhakikisha linashughulikia ipasavyo tatizo la kukatika kwa umeme bila sababu za msingi na kuwapa taarifa wateja wake ikiwa kuna matengenezo yanafanyika yanayolazimu kukata umeme.
Katika kipindi cha hivi karibuni, maeneo mengi nchini yameshuhudia changamoto ya kukatika kwa umeme mara kadhaa, hali liyoibua maswali mengi kwa wateja wa huduma hiyo nchini na kuzua mijadala mingi kwenye mitandao ya kijamii wengi wakihoji chanzo cha tatizo hili.