Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli, ameahidi kufikisha umeme katika vijiji 2600 nchini ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo.
Magufuli amesema hayo akiwa katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu Maswa mkoani Shinyanga, akiomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa rais kwa awamu ya pili.
“Hata umeme ulikuwa shida hapa Maswa, leo upo, wakati naingia madarakani vijiji vilivyokuwa na umeme Tanzania nzima vilikuwa 2018, kwa miaka mitano tumesambaza umeme vijiji 9570, Nchi ina vijiji 12,228 kwahiyo tumebakiza vijiji 2600, si mnipe tena miaka mitano nimalizie vijiji vilivyobaki”- amesema Magufuli.
“Tumejenga Barabara hapa Maswa panapendeza, tatizo la maji tutalimaliza, watoto wanasoma bila ada, hata Ulaya wanalipa ada ila sisi ni Bure,tumejipanga miaka 5 ijayo kuendelea kuboresha huduma za jamii, tutatoa elimu bila malipo, kuboresha afya na kadhalika ” ameongeza Magufuli.