Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema umeme sio anasa bali ni hitaji la lazima kwa wananchi na kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza kasi ya kujali shida za Watanzania, kwani anatatua changamoto mbalimbali likiwemo suala la umeme.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati wa hafla wa uwashaji umeme Kijiji cha Mubaba na Nyantakara vilivyopo Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera, huku akiwataka Wananchi kulinda miundombinu ya umeme ikiwemo Nguzo na mafuta ya Transfoma.
Amesema, “nimewaambia REA pelekeni umeme vijijini, tunataka Watanzania wazoee umeme. Umeme sio anasa tena bali ni hitaji la lazima kwa Watanzania, lakini pia wananchi watunze miundombinu ili umeme huu ufike maeneo mengine.”
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini – REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema Mkoa wa Kagera una jumla ya vijiji 662 ambapo vijiji 512 sawa na asilimia 77.3% vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya awali huku REA ikitekeleza jumla ya miradi mitano katika maeneo tofauti ya mkoa wa Kagera.