Kitengo cha mawasiliano Serikalini Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kimetoa ufafanuzi wa tukio la kukatika kwa umeme katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati wa mchezo wa Robo Fainali Mkondo wa Pili, Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Young Africans dhidi ya Mabingwa wa Nigeria Rivers United.

Timu hizo zilikutana jana Uwanjani hapo, lakini zililazimika kusubiri kwa zaidi ya dakika 15, baada ya umeme kuzimika wakati wa kipindi cha kwanza cha mchezo huo, ambao umemtoa mshindi wa jumla kwenda Hatua ya Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha mawasiliano Serikalini Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na kusainiwa na Eleuteri E. Mangi imeeleza:  Itakumbukwa 28 Machi, 2023 kulikuwa na mechi baina ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda (Uganda the Cranes) kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Siku hiyo umeme ulikatika wakati mechi hiyo inaendelea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kufuatia hali hiyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, (Mb) alimuelekeza Naibu Waziri Mhe. Hamis Mwinjuma, (Mb) kukaa na wataalamu kuchunguza tatizo la kukatika umeme katika uwanja huo hasa wakati mechi zinaendelea kuchezwa na kupata suluhisho la tatizo hilo.

Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, (Mb) alipokea taarifa ya wataalamu wa umeme ambao walimueleza kuwa chanzo cha hitilafu ya kukatika kwa umeme Uwanja wa Benjamin Mkapa ni kutokana na mchanganyiko wa umeme wa jenereta na umeme wa gridi ya taifa katika kuwasha taa za uwanja huo na wakapendekeza kuwa taa hizo ziwashwe na umeme wa jenereta pekee.

Mapendekezo hayo ya wataalam yalitekelezwa kama walivyoshauri.

Hata hivyo, hitilafu ya kuzimika kwa taa imejitokeza tena usiku wa leo wakati ya mechi ya Yanga na Rivers United ya Nigeria ambayo ni mechi ya robo fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Kutokana na kujirudia kwa hali hiyo licha ya ushauri wa wataalam kufuatwa, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, (Mb) ameagiza hatua zifuatazo kuchukuliwa.

1. Kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi watumishi wanaohusika na uendeshaji wa uwanja. Kufuatia agizo hilo na kwa mamlaka aliyonayo, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amewasimamisha kazi watumishi wafuatao ili kupisha uchunguzi,

i. Salum Mtumbuka – Kaimu Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

ii. Manyori Juma Kapesa – Mhandisi wa Umeme wa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

iii. Tuswege Nikupala – Afisa Tawala Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Aidha, Katibu Mkuu Bw. Saidi Yakubu amewasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi watumishi wafuatao ambao nao wana majukumu ya uendeshaji wa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

i. Gordon Nsajigwa Mwangamilo

ii. Gabriel Mwasele

iii. Yanuaria Imboru

iv. Dkt. Christina Luambano

2. Kufuatia hatua zilizochukuliwa, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amemteua Bw. Milinde Mahona kuwa Kaimu Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa na uteuzi huo unaanza mara moja kuanzia tarehe 01 Mei 2023.

3. Katibu Mkuu kuwasiliana na wadau wote husika ili mechi zitakazochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa zichezwe wakati wa alasiri/jioni badala ya usiku katika kipindi ambacho wizara ianakamilisha taratibu za kupata mzabuni atakayefanya ukarabati mkubwa katika uwanja huo kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa ligi/michuano ya kimataifa.

4. Ameagiza mamlaka za nje ya Wizara kufanya uchunguzi wa kukatika umeme katika uwanja huo na hatua za kuchukua.

Wizara inaomba radhi mashabiki wa soka nchini hususan wa timu ya Young Africans kwa kadhia iliyojitokeza.

Wizara inawaahidi Watanzania wote kwamba itaendeea kufanya ukarabati mdogo na mkubwa ili Uwanja wa Benjamin Mkapa uendelee kutoa huduma na burudani stahiki kwa Watanzania pamoja na nchi jirani zinazotumia uwanja huo.

Mkanganyiko kujiuzulu kwa Meja Jenerali Nyagaya
DC Malisa awataka Watanzania kuliombea Taifa