Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amewapa saa sita Shirika la Umeme Tanzania – TANESCO, kuirejesha katika hali ya kawaida ya uzalishaji mitambo iliyopata hitilafu katika kituo cha Ubungo I.
Kapinga amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua hali ya uzalishaji wa umeme katika Vituo vya Kupoza na Kusambaza Umeme vya Ubungo I na Ubungo II, ili kuona hali ya uzalishaji katika vituo hivyo, Septemba 29, 2023 jijini Dar es salaam.
Amesema, kutokana na changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini, ni vyema TANESCO wakaweka mpango wa kufanya marekebisho ya muda mfupi, wakati na muda mrefu katika mitambo, na marekebisho hayo yafanyike kwa wakati na muda sahihi, ili kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa watanzania wanapata umeme wa uhakika wakati wote.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshatoa maelekezo kuwa matengenezo yafanyike na ndani ya miezi sita yakamilike, sisi kama Wizara tunasimamia na kuhakikisha kuwa kila mashine ambayo inatakiwa kufanyiwa marekebisho inafanyiwa marekebisho hayo na yanamilika kwa wakati,” alisema Kapinga.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri huyo amekagua kituo cha Ubungo II chenye mitambo mitatu ambapo kati ya hiyo uko kwenye matengenezo na Katika kituo cha ubungo I chenye mashine 12, ambapo sita zinafanya kazi na nyingine ziko kwenye matengenezo.
@ Kwa hisani ya Zuena Msuya.