Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka wazazi kuwasimamia watoto katika matumizi ya vifaa vya kieletroniki ili kuwaepusha kujiingiza katika vitendo vya ngono na ukatili.
Ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yanayoadhimishiwa Juni 16 kila mwaka.
Ameongeza kuwa katika kipindi hiki watoto wamekuwa wakitumia vifaa vya kielektroniki ikiwa pamoja na simu na kompyuta, kujifunzia ni vyema watoto wazingatie matumizi sahihi ya vifaa hivyo ili kuepusha kufanyiwa vitendo vya kikatili.
“Katika eneo la malezi ya watoto wetu bado kuna changamoto kubwa ya matumizi ya mitandao tuhakikishe tunawasimamia watoto wetu wasijiingize katika masuala yasiyofaa katika mitandao hiyo” amesema waziri Ummy
Aidha ameitaja Mikoa ya kipolisi iliyoongoza kuwa na matukio mengi zaidi ya ukatili dhidi ya watoto kwa mwaka 2018 kwa ni Mkoa wa Tanga (1,039), Mbeya (1,001), Mwanza (809) na Arusha (792) na kwa mwaka 2019 ni Mkoa wa Tanga (matukio 1,156), Mkoa wa Kipolisi-Temeke (844), Mbeya (791) na Mwanza (758).
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Mtoto Sebastian Kitiku amewasisitiza wazazi kuwajibika kwa kuhakikisha wanawasimamia watoto na kufuatilia masuala ambayo yanaweza kusababisha ukatili kwa watoto.
Kauli mbiu ya Mtoto wa Afrika mwaka 2020 ni “Mifumo Rafiki ya Upatikanaji Haki ya Mtoto: Msingi Imara wa Kulinda Haki Zao”