Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu ameagiza Halmashauri ambazo zimekusanya mapato chini ya asilimia 75 ya makisio yake kufanya tathmini na kuhakikisha inaweka mikakati madhubuti ya kufikia malengo yao ifikapo 30 Juni, 2021.

Akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kipindi cha Julai, 2020 hadi machi, 2021, Ummy amesema kila Halmashauri ihakikishe inatumia kwa usahihi mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na mifumo ya uhasibu ili kutoa taarifa kwa kufuata matakwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma (IPSAS).

Waziri Ummy ameiagiza Mikoa kuendelea kusimamia, kutoa ushauri na maelekezo kuhusu suala zima la ukusanyaji na matumizi ya mapato ya ndani ya Halmashauri kabla ya viongozi wa juu kubaini matatizo ya halmashauri nchini.

Amezielekeza Halmashauri zote nchini kuzuia na kudhibiti matumizi ya fedha mbichi kabla makusanyo hayajapelekwa benki, kwa kuwa kwa mujibu wa sheria fedha inatakiwa kukusanywa na kupelekwa benki ndipo kuanza kutumika.

Waziri Ummy amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri kuacha kutumia fedha mbichi za makusanyo kabla ya kupelekwa benki na atakayekiuka hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwa kuwa atakuwa amekiunka miongozo ya kifedha inayomtaka kuhakikisha wanankusanya na kupeleka benki ndipo kuanza kutumika.

Ameielekeza Mikoa kuendelea kusimamia Halmashauri kwa kutoa taarifa kupitia mifumo ya kielektroniki, kusisitiza usuluhishi wa taarifa na usahihishaji wa takwimu katika mifumo mbalimbali na kuongeza jitihada katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Hata hivyo, amezitaka Sekretarieti za Mikoa kuhakikisha wanatoa ushauri stahiki kwa wakati, kutatua changamoto zilizopo katika suala zima la ukusanyaji wa mapato katika halmashauri wanazoziongoza, kutoa miongozo kwa lengo za kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinafanya vizuri katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Jafo awapa Wakurugenzi mwezi
Wakurugenzi Halmashauri 4 kikaangoni