Serikali kupitia Wizara ya Afya, imewatadharisha watanzania juu ya kuwapo virusi vya ugonjwa wa mafua ya ndege ambao ni hatari.
Aidha, ugonjwa huo umegundulika kuwapo nchi jirani ya Uganda ambapo taarifa zianasema kuwa maeneo yaliyoathirika ni yale yanayozunguka Ziwa Victoria.
Tahadhali hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, amesema ugonjwa huo umegundulika baada ya kuwapo kwa vifo vya ndege pori wengi katika maeneo ya Lutembe Beach, Masaka,Kachanga, Bukibanga na Bukakata nchini Uganda.
Amesema ingawa mpaka sasa hakuna binadamu aliyeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo nchini Uganda, tahadhali inatolewa kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kusambaa kwa binadamu ikiwa hatua madhubuti za kujikinga hazitazingatiwa.
“Kwa kuwa binadamu huweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa kugusana na ndege au kinyesi cha ndege aliyeathirika na ugonjwa huu, ni muhimu kutokugusa mizoga ya ndege pori au kinyesi chake,”amesema Ummy.
Hata hivyo, Ummy amewataka wananchi watoe taarifa iwapo wataona dalili zozote za ugonjwa huo na vifo katika jamii ya ndege wa kufugwa na ndege pori.