Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Ummy Mwalimu amewaonya wakurugenzi wote wa halmashauri watakaokaidi agizo la serikali la kutenga asilimia Nne (4) kwa ajili ya wanawake na vijana pamoja na asilimia mbili (2) kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mkoani Rukwa ambapo alipokea malalamiko kadhaa kutoka kwa wanawake walioshiriki kilele hicho kuhusu utoaji mdogo wa mikopo na wengine kutopata kabisa mikopo hiyo kutoka kwa halmashauri zao.
Ummy amewaagiza wakurugenzi wa halmashuri zote nchini kutenga asimilia hizo pamoja na kutoa mikopo yenye tija itakayoweza kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi na sio kurudi nyuma kiuchumi.
“Mikopo ya laki tatu haina tija toeni mikopo yenye tija itakayoendana na kauli mbiu ya kuelekea uchumi wa viwanda” alisema Ummy.
Ummy ameongeza kuwa ili kufikia azma ya Tanzania ya Viwanda basi halmashauri hazina budi kujiwekea mikakati ya kutoa mikopo mikubwa itakayo wawezesha wanawake na wananchi kwa jumla kufikia dhana hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kalembo, Julieth Binjula ameiomba Serikali kuendelea kuwawezesha wanawake kwa kuwapa elimu ya jinsi ya kutumia fedha na kuendesha miradi mbalimbali itakayo wakwamua kiuchumi.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Khalfan Haule amesisitiza wadau kushirikiana na Serikali pale ambapo wanaweza kuwawezesha wanawake sehemu walipo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kutoa mchango katika kuchangia kujiletea maendeleo jumuishi.
Siku ya Wanawake Duniani 2018 kilele chake ni siku ya tarehe 8 Machi, na Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa ni ‘‘KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA: TUIMARISHE USAWA WA JINSIA NA UWEZESHAJI WA WANAWAKE VIJIJINI”.
Ummy amesema, dhamira ya wizara nikuona kila mdau mmoja mmoja anaelewa madhumuni ya kauli mbiu na kuchukua hatua kuchangia utekelezaji wa jumbe mahususi wa kuwajumuisha wanawake wa vijijini katika maendeleo yao na ya Taifa kwa jumla.