Umoja wa Afrika umelaani mashambulizi ya angani yaliyofanywa katika kituo cha wakimbizi nchini Libya yaliyosababisha vifo vya watu 40.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat ametaka uchunguzi huru ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya waliohusika na uhalifu huo wa mauaji.
Mashambulizi hayo yanahusishwa na mbabe wa kivita nchini Libya, Khalifa Haftar ambaye amekuwa akijaribu kwa miezi mitatu kuukamata mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.
Aidha, mashambulizi hayo yamefanyika jana katika kituo cha wahamiaji kilichopo katika mji mkuu wa nchi hiyoTripoli. ambapo takriban watu 70 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo.
Msemaji wa huduma za dharura nchini Libya, Osama Ali ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hiyo ni tathmini ya awali na idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka.
Hata hivyo, ameongeza kuwa wahamiaji 120 walikuwa wanashikiliwa katika jengo la kuhifadhi ndege ambalo lilishambuliwa.