Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo leo Aprili 30, 2020 kwa nyakati tofauti wamezungumzia taarifa zilizokuwa zimeenea kuhusu afya ya Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un.
Pempeo amewaambia waandishi wa habari kuwa vyombo vya Marekani havijamuona Kim katika siku za hivi karibuni lakini wanafuatilia kwa karibu taarifa kuhusu afya yake. Pia, Pompeo alidai kuna taarifa za kutokea njaa katika nchi hiyo.
“Hatujamuona. Hatuna taarifa yoyote ya kuwaeleza leo kuhusu Kim Jong-un, lakini tunafuatilia kwa karibu sana,” alisema Pompeo.
“Kuna hatari kuwa kutakuwa na njaa, uhaba wa chakula ndani ya Korea Kaskazini pia. Tunafuatilia kila kitu kwa karibu, kwakuwa hayo yote yana madhara katika mpango wetu, ambao ni kuhakikisha tunaondoa mpango wa nyuklia nchini humo,” Pompeo aliiambia Fox News.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Guterres amewaambia waandishi wa habari kuwa hawana taarifa yoyote kuhusu hali ya kiongozi huyo.
“Sisi hatuna taarifa yoyote ya kinachoendelea kuhusu Kim Jong-un,” Guterres aliwaambia waandishi wa habari.
Kulikuwa na tetesi kuwa afya ya kiongozi huyo wa Korea Kaskazini imezorota baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo ambao haukwenda vizuri, taarifa nyingine zikadai kuwa huenda amefariki dunia.
Hata hivyo, Mshauri wa Rais wa Korea Kusini kwenye masuala ya Sera za kimataifa aliiambia CNN kuwa wanaamini Rais huyo wa jirani zao ni mzima wa afya njema. Alisema kuwa hakuna hali yoyote tofauti inayoonekana nchini humo.
Saa chache baadaye, Shirika la Habari la Korea Kaskazini lilitangaza kuwa Kim Jong-un ameishukuru timu ya wataalam waliojenga kituo cha utalii kipya na cha kisasa nchini humo.