Sakata la kupotea kwa Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben Saanane limechukua sura mpya mara baada ya Umoja wa Mataifa kusema upo teyari kutuma watu nchini kwa ajili ya uchunguzi.
Saanane ambaye pia ni Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 18 mwaka jana mpaka sasa haijaeleweka alipo.
Siku chache baada ya kutoweka kwa Ben Saanane, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliitaka Serikali ifanye uchunguzi wa kina kuhusu kupotea kwake.
Wakati utata huo wa kupotea kwa Ben Saanane ukiendelea, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu duniani ya UN yenye Makao yake Makuu Jijini Geveva Uswisi, imesema iko tayari kutuma timu ya watu kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina.
Aidha, uamuzi huo umefikiwa katika mkutano ulioitishwa na Ofisi hiyo wa Kanda ya Afrika uliohusisha nchi za Sudan, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Ethiopia, Djbouti na Tanzania.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Hellen Kijo-Bisimba, amesema suala hilo liliibuka baada ya wajumbe wa mkutano huo kutaka kujua kiundani wa sakata hilo, lakini hakukuwa na taarifa za kina.
“Wajumbe walionyesha kuguswa na jambo hilo, la mtu kupotea katika mazingira ya kutatanisha na kutaka tueleze kiundani zaidi ilivyokuwa, hatukuwa na taarifa za kina hivyo wakasema wako tayari kulifanyia kazi endapo tutatuma taarifa ya dharura,”amesema Bisimba.
Hata hivyo, Kamishna wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz alipotafutwa kueleza kuhusu maendeleo ya uchunguzi alisema yupo kwenye kikao hivyo asingeweza kuongea chochote kuhusu suala hilo.