Na Mwandishi wetu, New York

Umoja wa Mataifa umeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango wake wa kulinda amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi.

Katika mazungumzo hayo, wamegusia masuala ya maendeleo katika ukanda wa maziwa makuu, ikiwa ni pamoja na hali ya kisiasa ya Burundi na usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema umoja huo unatambua mchango na jitihada za Tanzania na kuongeza kuwa wapo tayari kushirikiana na Tanzania katika jitihada zake za kuzuia matukio yanayosababishwa na makundi ya waasi na wenye misimamo mikali.

Kwa upande wake Prof.  Kabudi ameuhakikishia Umoja wa Mataiafa kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja huo katika vikosi vya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na sehemu nyingine duniani ili kuufanya Ukanda wa Maziwa Makuu, Afrika na duniani kwa ujumla kuwa mahali salama pa kuishi.

Ameongeza kuwa Tanzania inaunga mkono mabadiliko yanayofanyika ndani ya Umoja wa Mataifa na kwamba inakubaliana na mabadiliko hayo.

Aidha, Waziri Kabudi ameitumia fursa hiyo kumueleza katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa hatua mbalimbali za kimaendeleo ambazo Tanzania inatekeleza katika kufikia malengo ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa.

Katika tukio jingine Tanzania imesaini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia na kuwa mojawapo ya nchi kumi na mbili zilizosaini na kuridhia Mkataba huo.

Pia, hatua hiyo imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 60 zilizosaini na ya 32 kati ya nchi zilizoridhia kuanza kutumika kwa mkataba huo.

Prof. Kabudi amesema kuwa Tanzania inaunga mkono jitihada zote za kupiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia kama sehemu ya kuufanya ulimwengu kuwa salama ambapo chini ya mkataba huu zimefanywa kuwa silaha za maangamizi.

Hata hivyo Prof. Kabudi amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikatai na inaunga mkono matumizi ya amani ya nguvu za nyuklia kama sehemu ya dawa, kuhifadhi vyakula na uzalishaji wa nishati miongoni mwa matumizi mengine chini ya uangalizi madhubuti wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki.

Ameongeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua hiyo ikitilia maanani kuwa zipo nchi zenye silaha za nyuklia na zimetenga bajeti kubwa kwa ajili ya kuimarisha silaha hizo.

Alitoa wito kwa mataifa hayo kujenga imani kwa mataifa mengine na kwamba matumizi ya silaha hizo si njia sahihi na salama za kuihakikishia dunia amani na usalama.

Prof. Kabudi anatarajiwa kuhutubia katika mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baadae hii leo jijini New York, Marekani.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 30, 2019
Mambo 10 kushangaza usiyoyajua kuhusu Kuku