Makundi ambayo ni Wakala wa Umoja wa Mataifa (UN), yametoa tamko la pamoja kupinga vikali vitendo vya upimaji wa ubikira vinavyofanywa kwa wanawake na wasichana katika nchi zaidi ya 20.
Zoezi la upimaji wa bikira limeripotiwa kufanywa kwa lengo la kubaini kama mwanamke hajawahi kushiriki tendo la ndoa au la, ambapo hali ya kuwa bikira imekuwa ikichukuliwa kama ukamilifu wa msichana unaoongeza thamani ya mahari yake wakati wa kuolewa.
Kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya Umoja wa Mataifa, nchi zaidi ya 20 zimebainika kufanya tukio hilo ambapo hufanyika kwa uwazi kwa kutumia vidole, hali ambaye imetajwa na madaktari kuwa ni hatari kwa afya ya mhusika.
Katika hatua ya kuhuisha vita ya kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana duniani kote, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayoshughulikia haki za binadamu, afya pamoja na wanawake, (UN Human Rights Office, UN Women na World Health Organisation), yamesema kwenye tamko lao la pamoja, “vitendo hivi ambayo havina maana kiafya, na ambavyo huongeza maumivu, kudhalilisha na kutesa kisaikolojia lazima vikome.”
Tamko hilo limefafanua kuwa hakuna vipimo ambavyo vinaweza kueleza kama mwanamke au msichana amewahi kufanya mapenzi au la kwa namna hiyo, kwani maumbile ya mwanamke hayawezi kutoa uthibitisho huo kwa uhakika kiuhalisia.
Wameeleza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha haki za binadamu na huathiri maendeleo ya mwanamke kiakili, kimaumbile na hata kijamii.
Ingawa imedaiwa kuwa vitendo hivyo hufanywa na jamii nyingi duniani, ripoti ya UN imethibitisha nchi 20 ambazo utaratibu huo umegeuzwa kuwa utamaduni.