Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuanza mazungumzo ya maandalizi kuhusu uhusiano wa kanda hiyo na Uingereza baada ya Brexit, licha ya kusisitiza kuwa hakuna hatua muhimu zilizopigwa katika mazungumzo hayo.

Rais wa Baraza hilo, Donald Tusk ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twita kuwa viongozi 27 wa umoja huo waliokutana jijini Brussels wamekubaliana kuanza maadalizi ya mazungumzo ya kufanya biashara na Uingereza.

Aidha, kiongozi mwenye nguvu na ushawishi mkubwa katika umoja huo, Angel Merkel amesema kuwa anachotaka ni makubaliano ya wazi na siyo tu suluhu isioyatabirika, huku akisisitiza kuwa Uingereza laazima itimize wajibu wake wa kifedha.

“Tunatumaini kwamba kufikia Desemba mwaka huu tutakuwa tumepiga hatua za kutosha kuwezesha awamu ya pili ya mazungumzo kuanza, lakini hiyo inategemea umbali gani Uingereza itakuwa imefikia ili tuweze kusema kwamba inatosheleza juu ya masuala makuu ya awamu ya kwanza,” amesema Merkel.

Hata hivyo, Umoja wa Ulaya umesema kuwa katika masuala makuu matatu ya kutengana na Uingereza yaliyojadiliwa, ni suala kuhusu haki za binadamu ndilo lililojadiliwa bila mabishano, huku masuala ya ushiriki wa Uingereza katika biashara na mipaka kati ya Ireland ya Kaskazini na Ireland yakizidi kuleta mabishano.

 

Zitto Kabwe: Serikali ilikosea kujitangazia ushindi
Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 21, 2017